“Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na
adabu” (Mithali 1:7).
“The fear of the Lord is the beginning of knowledge; fools despise wisdom and
instruction” (Prov. 1:7 ESV).
Kuna
jambo zuri la kujifunza hapa leo. Nitatumia mfano. Wakati wa vita kuna mambo
mawili yanaweza kusababisha ushindi. Jambo la kwanza ni SILAHA na jamabo la pili ni
MBINU za vita.
Siku
zote ushindi wa vita hautegemei UBORA wa silaha peke yake. Na kwa upande
mwingine, UTENDAJI wa silaha hautegemei mtu anayetumia ila NGUVU iliyoko nyuma
ya huyo MTU. Kwa mfano, Goliath alikuwa na SILAHA bora na kali kuliko Daudi,
pia Goliath alikuwa Jemadari na mzoefu wa vita. Tofauti ya Goliath na Daudi
ilikuwa (1). Nguvu iliyokuwa nyuma yao,
na (2). Maarifa katika Mungu (Knowledge of God).
Siku
zote Daudi akisikia Vita, alikuwa anasema
“hawa wanataja magari na farasi (silaha), ila mimi nitalitaja Jina la Bwana”. Sasa
usidhani Daudi alikuwa habebi upanga, Daudi alikuwa anabeba upanga kama
wenzake, ila HAKUUTEGEMEA upanga wake. Alijua
siri ya USHINDIni katika mambo mawili: Kumjua
Mungu wake na Nguvu za Mungu wake.
Hebu
tuangalie kumcha Mungu ni kitu gani. Ukitaka kujua kipimo cha UCHA MUNGU wako,
zingatia hapa, “the fear of the Lord”.
Jiulize, ni kwa kiwango gani “una hofu ya Mungu” ndani yako? Yesu
alipokuja, hakutaka kupingana na Torati, na wala hapingani nayo, ila ilitaka
watu wamjue BABA kwa namna ya tafauti na walivyomjua mwanzo. Hebu angalia
hapa, “Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika
torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na
kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya
pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi
yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote
na manabii” (Mat. 22:35-40).
Kuna
tofauti ya HOFU ambayo imejikita katika “UPENDO”
na HOFU iliyojikita katika “HUKUMU”.
Ukiona HOFU inayokufanya usifanye “JAMBO” fulani lolote inatokana na kuogopa HUKUMU, yaani lawama, adhabu,
kushangaliwa, sheria ya nchi, nk., hiyo SIO hofu ya Mungu ila ni HOFU ya HUKUMU. Watu wengi wameenenda kwa namna fulani
kwa kuogopa (kuwa na hofu ya wanadamu) JAMII inayowazunguka, na wala sio
Mungu wao! Mchamungu siku zote
kinachomsukuma kutofanya jambo, au kufanya kitu, ni UPENDO kwa Mungu wake.HOFU ya kumtenda
Mungu dhambi, au KIU ya kumpendeza Mungu ndio inayomsukuma kufanya jambo fulani
au kuacha kufanya jingine. Mtu wa namna hii anaitwa “mchamungu”.
Hebu
angalia tena hapa, Yesu “Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo
wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo
kuu, tena ni ya kwanza.” Hii ni AMRI kuu. Ukifika mahali pa KUMPENDA Mungu kwa moyo wako wote (katika
kuwaza kwako), roho yako yote (uhai wako sio kitu kuliko kumkosea Mungu wako),
akili zako zote (maamuzi yako, matendo yako, nk.), hii ni hali ya JUU
kabisa ya KUMCHA Mungu. Angalia tena, “Mpende
Bwana Mungu wako”, kinachokusukuma ni“UPENDO”
sio “HUKUMU”. Zingatia hapa “Bwana
Mungu WAKO”, sio “WENU”. Ikifika
mahali pa mtu na Mungu, hakuna “ujumla”,
ni wewe na “Mungu wako”. Kila mtu atasimama kama yeye na sio “nyie”. Ndio maana
unatahadharishwa “angalia mtu
asijekuitwaa taji yako”. Taji “yako”, utaipigania wewe mwenyewe na sio
kiongozi wako kanisani, wala mzazi au mke/mume, ni wewe na Mungu.
Kuna
tofauti ya mtu anayempenda Mungu kwa sababu anampenda Mungu, na mwingine
anampenda Mungu kwa hofu ya JEHANAM. Anayempenda Mungu kwa sababu anampenda
Mungu huangalia kumpendeza Mungu bila kutarajia “malipo”, any form of reward. Yaani hawezi kufika mahali
akalinganisha kuanguka, kushindwa, majanga, nk., na MUNGU kuwa kinyume chake.
Anayempenda Mungu kwa kuogopa JEHANAM, siku zote utamsikia akiwa busy na
kutumia NGUVU kupambana na dhambi. Na kwa sababu yuko busy kupambana na dhambi,
katika maisha yake DHAMBI ni dhahiri kuliko UTAKATIFU. Ndio maana utamwona siku zote anahesabu na kushangaa
dhambi za watu wengine na kujihesabia haki tu. Mtu anayempenda Mungu kwa sababu
anampenda Mungu, dhambi sio option
katika maisha yake kwamba afanye au asifanye, moyoni mwake hana uchaguzi kwa
maana hatamani hiyo dhambi. Huwezi kupambana na kitu usichokitamani. Ukimpenda
Mungu sana, moja kwa moja unajikuta unakuwa MSHINDI, na ukisikia mtu ameanguka dhambini, inakuuma kama vile
wewe ndio umeanguka, na ule UPENDO utakusukuma kuwaombea wengine na sio
kuwasengenya na kuwasema tu.
Hebu
angalia hapa, “atendaye dhambi ni wa
Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi
hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila
mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa
ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na
Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao.
Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda
ndugu yake.” (1Yoh. 3:8-10). Dunia imewafikisha watu mahali pa kusahau
kwamba Mungu ni Mtakatifu sana, hofu imegeuka kuwa “hofu ya dhambi (hukumu)” na
wala sio “hofu ya Mungu”. Paulo
alifika mahali akasema “sheria inawahusu wakosaji”, yaani kama wewe ni “mwana
wa Mungu”, sheria ya “usizini”, “usiibe”, nk., haikuhusu kwa sababu , huna
“kiu” na hiyo dhambi. Ukiangalia hapo katika 1Yohana 3:8-10, utaona Yohana pia amesisitiza UPENDO. Msingi wa
hili fundisho la Yohana ni KUMPENDA Mungu na ndugu yako (watu wengine).
Angalia
hapa, “Naye akashika kigae cha
kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa
washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia,
Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema
mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu
hakufanya dhambi kwa midomo yake” (Ayubu 2:8-10). Mtazamo ya mke wa
Ayubu ulikuwa, kufanikiwa ndio “nguvu” ya kumcha Bwana. Ayubu alijua kwamba “hakuna uhusiano kati ya majaribu, magumu,
shida, nk, na UTIMILIFU au UCHA MUNGU wake”, katika shida na raha,
alimheshimu Mungu kiasi cha kupata shida hata akifikiri tu kwamba “labda”
watoto wake wanatenda dhambi huko, licha ya yeye mwenyewe, na ilimpasa “atoe
sadaka” kwa ajili yao, ili Mungu awarehemu tu, japo hana uhakika kama wanatenda
dhambi au la. Huu upendo hauwezi
kukuruhusu UKAMSENGENYA ndugu yako aliyeanguka dhambini, utasimama na kuomba
rehema ili Mungu amtegemeze asianguke tena. Hii ni moja wapo ya sifa za
wachamungu, kutegemezana na sio kuangushana au kuchekana kwenye kushindwa.
Nikirudi
katika kumchamungu, faida zake ni nyingi. Moja wapo niudhihirisho wa Mungu maishani mwako. Jinsi unavyozidi kumcha Mungu,
na kumpendeza, ndivyo utazidi kumwona, na HOFU ya Mungu itaongezeka. Angalia
tena hapa “Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo
mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa
panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango
la mbinguni” (Mwa. 28:16-17). Baada ya Yakobo kupokea baraka, na
kuwatii wazazi wake (kwa sababu hakuoa Wakanani (wamataifa) kama Esau ndugu
yake), Mungu aliendelea kumbariki na kujidhihirisha kwake. Angalia tena hapa, “Kweli
BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua”! Yakobo anashangaa kwamba
“kumbe” Mungu yuko hapa na hakujua. Angalia tena hapa, “Mahali hapa
panatisha kama nini!”hofu ya Mungu ilishuka juu yake zaidi kuliko
mwanzo, na ukisoma mistari inayofuata akasukumwa na kutoa SADAKA (fungu la kumi
la mali zake) pia. Hofu ya Mungu ambayo
Msingi wake ni Upendo KWA Mungu, itakusukuma kumtii Mungu, kwa sababu
unamwogopa Mungu na sio kwa sababu unaogopa Dhambi au HUKUMU. Na hii ndio
maana ya kuwa mchamungu.
Mungu
akubariki sana, endelea kuwa nasi kwa makala mbalimbali.